Huenda mvutano katika Shamba lenye utata la Waitiki ukachukua mkondo mpya baada ya wakazi watatu wanaotoka katika eneo bunge la Likoni, kuwasilisha kesi mahakamani wakitaka mahakama kuizuia serikali kumlipa Evanson Waitiki, mmliki wa shamba hilo.
Walalamishi hao, Abdhala Juma, Juma Athmani na Salim Mohammed walidai kuzaliwa katika shamba hilo na kwamba wanamiliki ekari nne ya shamba hilo lenye ekari 930.
Watatu hao walisema Waitiki hafai kulipwa hadi kesi hiyo itakaposikizwa na kuamuliwa.
Kupitia wakili wao Mogaka Omwenga, watatu hao wamewasilisha kesi hiyo katika mahakama kuu ya Mombasa na kuitaja kuwa ya dharura huku wakiwajumuisha waziri wa ardhi Jacob Kaimenyi na mwanasheria mkuu Githu Mwigai kama wahojiwa.
Haya yanajiri wakati serikali tayari imekubali kununua shamba hilo ili kuigawanya kwa maskwota 11,000 ambao wamekuwa wakiishi katika shamba hilo bila vibali.
Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuongoza awamu ya kwanza ya shughuli ya utoaji hata miliki 5,0000 kwa maskwota wanaoishi katika shamba hilo siku ya Jumamosi, katika uwanja wa Caltex Likoni.
Hata hivyo, baadhi ya wakaazi wameapa kususia shughuli hiyo wakidai kunyanyaswa kufuatia hatua ya mratibu wa ugavi wa shamba hilo Joseph Kanyiri, kusema kuwa watalazimika kulipa Shilingi elfu 182 kabla ya kukabidhiwa hati miliki.