Share news tips with us here at Hivisasa

Wafanyibiashara na wakazi kutoka eneo la Mwembe Tayari wamelalamikia kunyanyaswa na maafisa wa polisi nyakati za asubuhi.

Wakizunguza na mwandishi huyu siku ya Alhamisi, wakaazi hao walisema kwamba maafisa wa polisi hufika kila asubuhi katika vituo vya mabasi ya kuelekea mjini Nairobi na kukamata yeyote anayetembea katika eneo hilo.

Kwa upande wao, wafanyibiashara katika eneo hilo walisema kwamba hali hiyo imewafanya kuogopa kufanya kazi nyakati za asubuhi kwani polisi huwakamata na kuwapeleka rumande.

Kulingana na mfanyibiashara mmoja anayefanya biashara ya kusafisha viatu ambaye hakutaka kutaja jina lake litajwe, lori la maafisa wa serikali ya kaunti wakishirikiana na wale wa serikali kuu huzunguka kila alfajiri na kuwabeba watu wote wanaotembea katika eneo hilo, bila ya kuzingatia kuwa wanatafuta riziki kwa njia halali.

Aidha, mfanyibiashara huyo aliwataka viongozi kuingilia kati na kulizungumzia swala hilo kwani wengi wao kwa sasa wanalazimika kutofika kazini mapema kama ilivyokuwa hapo awali.