Maradhi ya kipindupindu yameripotiwa kuzuka katika baadhi ya maeneo mjini Mombasa ambapo tayari visa 15 vimesajiliwa.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Kulingana na maafisa wa afya mjini humo, visa vinne vimeripotiwa katika eneo la Likoni huku maeneo ya Mvita, Kisauni na Changamwe yakiripoti visa sita, tatu na nne mtawalia.

Mwanamke mmoja na watoto wawili waliopelekwa katika kituo cha afya kilichoko Likoni wameripotiwa kuonekana na dalili za kipindupindu baada ya kulalamika kuumwa na tumbo na kichwa.

Hata hivyo, hali hiyo huenda ikadhibitiwa kwani madaktari wasio na mipaka tayari wameweka hema katika eneo la Vijiweni, Likoni ili kuwahudumia waathiriwa.

Kamishna wa kaunti dogo ya Likoni Rose Chege, aidha, amewaagiza machifu wote kuhakikisha kuwa kila boma linaimarisha hali ya mazingira na kusafisha vyoo vyao ili kuzuia ugonjwa huo kusambaa.

Mwaka jana, watu wengi waliathirika na hata wengene kuaga dunia baada ya maradhi hayo kuzuka mjini Mombasa.