Gavana wa Nakuru Kinuthia Mbugua amewaonya baadhi ya viongozi ambao wanadai lengo lake la kuanzisha mradi wa Gavana Mtaani ni siasa za kukampenia uchaguzi ujao ila si kutumikia wananchi.
Mbugua ameonyeshwa kughadhabishwa kwake na hatua hiyo huku akiwahakikishia wananchi kuendelea na mradi huo ili wapate kuwahudumia watu wa kaunti hiyo.
"Mradi huu si wa kisiasa namna inavyodaiwa na baadhi ya viongozi ambao nia yao ni kujinufaisha na kutenganisha wananchi. Sisi kama serikali tutaendelea kutumikia wananchi na kutimiza ahadi tulizotoa hapo awali." Mbugua alielezea.
Gavana huyo amekuwa akizungumza katika kaunti ndogo ya Rongai siku ya Alhamisi ambapo ameendeleza siku ya pili ya mradi huo wa Gavana Mtaani katika eneo hilo.
Mbugua pia amewapa changamoto wanaoshuku kazi yake kujitokeza na kushuhudia kazi ambazo wametekeleza katika mradi huo.
"Wale ambao wanashuku kazi yetu ninawapa changamoto mje mshuhudie huduma ambazo tunatoa kwa wananchi badala ya kupoteza wakati mwingi na pesa za kusafiri kueneza jumbe ambazo hazifai. Tungali na mengi ya kutekeleza na kwamwe hatutakomea hapa hadi pale tutakapotimiza malengo yetu," Mbugua alielezea zaidi.
Mbugua aliambatana na viongozi mbalimbali katika kaunti hiyo akiwemo naibu wake Joseph Ruto miongoni mwa viongozi wengine. Mradi huo utaingia mkondo wake wa sita katika eneo la Subukia tarehe 16 na 17 mwezi huu.