Share news tips with us here at Hivisasa

Mbunge wa Lungalunga Khatib Mwashetani amewataka wakazi wa eneo zima la Pwani kutodanganywa na viongozi wabinafsi na kudharau miradi muhimu inayotolewa na serikali ilhali wao hawawezi kutekeleza miradi hiyo.

Akiongea na wanahabari huyo mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Mwashetani amesema kuwa japo serikali ina makosa yake, siyo kila kitu serikali inachofanya kwa wakenya kina makosa, na lazima maswala mengine yazingatiwe ili kuwafaidi wakenya wote kwa jumla.

Kulingana na Mwashetani, hatua ya mrengo wa Cord kupinga kila kitu serikali inachowatekelezea wakazi sio jambo bora, na viongozi wa ukanda wa Pwani wanafaa kushirikiana na kuwafanyia maendeleo wakazi badala ya kupiga domo kaya na kuikosa serikali huku wakazi wakizidi kuteseka.

“Wapwani wakati umefika sasa wa kufikiria mambo kwa makini kwa sababu viongozi walioko kwa sasa ni wabinafsi, na msipokuwa makini basi mtajikuta mmewachagua viongizi walafi na kamwe hawatawasaidia katika maswala ya maendeleo na kufanikisha ujenzi wa miradi mbalimbali mashinani,” alisema Mwashetani.

Shinikizo za kiongozi huyo zinajiri huku viongozi mbalimbali wa Pwani wakiwashinikiza wakazi wa eneo hilo kujitenga na mipango ya serikali kwani haiwasaidii na kuahidi kuwafanyia maendeleo bora iwapo watawachagua kuingia serikali wakati wa uchaguzi mkuu.

Picha: Mbunge wa Lungalunga Khatib Mwashetani katika mkutano wa kisiasa hapo awali. Amewataka wakazi wa eneo zima la Pwani kutodanganywa na viongozi wabinafsi na kudharau miradi muhimu inayotolewa na serikali. twitter