Madereva kutoka Kibera wameapa kutolipa ada ya kila mwezi kufuatia agizo la serikali ya Kaunti ya Nairobi kupiga marufuku kuingia katikati ya jiji la Nairobi.
Wakiongozwa na Michael Otengo, madereva hao waliikosoa serikali ya Kaunti ya Nairobi pamoja na Wizara ya Uchukuzi kwa kusema kuwa hatua hiyo itasababisha hasara kubwa kwa biashara yao.
Akizungumza siku ya Jumanne katika eneo la Laini Saba, Otengo alisema kwamba hali ambayo inashuhudiwa kwa sasa katikati mwa jiji ni pigo kubwa kwa biashara yao kama madereva.
“Hatua hiyo itatusababishia hasara kubwa na tumeamua kuwa hatutalipa ada ya kila mwezi kwa Kaunti ya Nairobi mpaka turuhusiwe kubeba abiria katikati mwa jiji kama ilinyokuwa hapo awali,” alisema Otengo.
Aidha, alisema kuwa agizo la Kaunti ya Nairobi ni kinyume na matarajio katika biashara yao kama madereva, na kuongeza kuwa sasa watalazimika kuongeza nauli kuingia na kutoka jijini Nairobi.