Idara ya usalama eneo la Pwani imeahidi kukabiliana kikamilifu na magenge ya kihalifu sawia na magaidi wanaolenga vituo vya polisi katika eneo hilo.
Hii ni baada ya kuvamiwa kwa kituo cha polisi cha Central mjini Mombasa, na wanawake watatu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa kundi la kigaidi la al-shaabab.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu, mshirikishi mkuu wa usalama eneo la Pwani Nelson Marwa, alisema kuwa oparesheni kali ya kuwasaka magaidi na kukabiliana nao itaendelezwa kuhakikisha kuwa usalama unaimarisha hata mashinani na sio tu katika vituo vya polisi.
"Tayari maafisa wa polisi wako kila mahali kuhakikisha kuwa usalama umeimarishwa ili kukabiliana kikamilifu na magaidi hapa pwani," alisema Marwa.
Marwa alisema kuwa maafisa wake watamkabili kikamilifu mtu yeyote mwenye nia potovu kama vile kutekeleza uvamizi wa kigaidi.
Kauli ya Marwa inajiri siku moja tu baada ya wanawake watatu kuuawa baada ya jaribio lao la kuvamia kituo cha polisi cha Central mjini Mombasa kutibuka.