Katibu mkuu wa Chuo Kikuu cha Nairobi Erick Janganya ametaka polisi kumwachilia huru mwenyekiti wa muungano wa wanafunzi wa SONU Paul Ongili al maarufu Babu Owino, ili kupunguza mvutano katika taasisi hiyo.
Babu alitiwa mbaroni na kupelekwa katika Kituo cha polisi cha Kilimani siku ya Jumatano usiku, siku chache baada ya chuo hicho kufunguliwa kufuatia kufungwa kwa muda mrefu kutokana na ghasia zilizozuka chuoni humo.
Bwana Janganya, ambaye bado anapinga kusimamishwa kwa masomo yake kwa muda, aliishutumu taasisi hiyo kwa kusababisha taharuki miongoni wa wanafunzi na kuutaka usimamizi wa chuo hicho kujitenga na maswala ya wanafunzi.
"Nimekuwa katika chuo hiki kwa muda mrefu na hunichukua siku kadhaa kubaini wanafunzi wanachokifikiria,” alisema Janganya.
"Kwa sasa hali ya taharuki imetanda na ningependa kuwarai polisi kumwachilia huru Babu ili wanafunzi waweze kurejelea masomo yao kwa amani,” alisema Janganya.
"Uongozi wa shule unafanya makosa kwa kujihusisha na maswala yetu. Masomo ya baadhi yetu yamesimamishwa kwa muda na tunapambana kwa ajili ya mustakabali wetu ilhali wanaendelea kututia mbaroni,” alisema kiongozi huyo.
"Tunataka wanafunzi kumaliza muhula vizuri bila uchochezi wowote na wasimamizi wa chuo hichi hawapaswi kutumia polisi kutishia mmoja wetu,” Janganya alimwambia mwandishi huyu kupitia njia ya simu.
Janganya ambaye pia ni kiongozi wa vijana wa chama cha ODM katika Kaunti ya Kisii aliipa taasisi hiyo changamoto kushirikisha wanafunzi moja kwa moja.
"Polisi waliwapiga wanafunzi hivi majuzi na sasa wanamkamata mtu ambaye anaelewa mfumo wa uongozi," alisema Janganya.
"Ni muhimu kwa uongozi wa taasisi hii kuacha kutumia polisi katika kusuluhisha mambo yetu. Babu anapaswa kuachiliwa huru ili kuwe na amani katika chuo hiki."