Share news tips with us here at Hivisasa

Chifu wa lokesheni ya Mwamonari, wadi ya Sensi Kaunti ya Kisii Titus Mochiemo amewaomba wakazi wa lokesheni hiyo kujitokeza kwa wingi siku ya Jumatatu juma lijalo ili kuwachagua wanachama wa polisi jamii (community policing) ambao watasaidia kuimarisha usalama katika vijiji mbalimbali vya lokesheni hiyo.

Uchaguzi huo utafanyika siku ya Jumatatu katika eneo la Sombogo, na kuomba wakazi kujitokeza kwa wingi ili kujichagulia wanachama hao wa polisi jamii.

Akizungumza siku ya Alhamisi katika sherehe ya mazishi yaliyoandaliwa katika eneo la Nyakeiri, chifu Mochiemo alisema hawataki wanachama hao wachaguliwe bila mapendekezo ya wananchi wa lokesheni hiyo, kwani katiba huruhusu wananchi kuhusishwa katika uchaguzi wa wanachama wa polisi jamii .

“Naomba kila mkazi wa lokesheni yangu ajitokeze siku ya Jumatatu wiki kesho katika eneo la Sombogo ili tuchague wanachama wa polisi jamii ambao walinda usalama katika vijiji vyetu tunavyoishi,” alisema Mochiemo.

Hapo mbeleni kamishena wa Kaunti ya kisii Chege Mwangi alivunjilia mbali vikundi vyote vya polisi jamii katika Kaunti ya Kisii kwa kile kilichosemekana kuwa wanachama hao walijifanya kuwa maafisa wa polisi huku kazi yao ikistahili kuwa ya kujulisha polisi kile kinachoendelea vijijini.

Mwangi alilazimka kuvunja vikundi hivyo na sasa wanachama wapya wameanza kuchaguliwa katika sehemu mbalimbali za kaunti ambao watafuata maagizo kando na kujifanya maafisa wa polisi.