Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kituo cha Mombasa Urban hatimaye kimepata OCPD mpya baada ya kukaa takriban mwezi mzima nafasi hiyo ikiwa wazi.

Kulingana na uteuzi mpya uliofanywa na Inspecta Mkuu wa Polisi Joseph Boinett siku ya Jumapili, Lucas Ogaro sasa ndiye OCPD mpya wa Mombasa.

Ogaro atachukua nafasi hiyo iliyoachwa wazi baada ya kifo cha aliyekuwa OCPD wa eneo hilo Martin Asin, aliyefariki kutokana na ajali ya barabarani.

Asin alikumbana na ajali mapema mwezi Machi mwaka huu, katika barabara kuu ya Mombasa-Nairobi alipokuwa akiendesha gari lake la kibinafsi kuelekea mjini Nairobi.

Katika mabadiliko hayo, Wachira Mathenge ameteuliwa kama kamanda mpya wa Kaunti ya Kilifi, nafasi iliyokuwa imeshikiliwa na David Kerina kwa muda wa miezi sita kama kaimu.

Mathenge aliyekuwa naibu kamanda katika msafara wa Rais Uhuru Kenyatta sasa atashughulikia majukumu mapya katika eneo hilo la Pwani.

Kerina aliyeshikilia nafasi hiyo ya kamanda wa Kilifi kama kaimu anatarajiwa kurejelea nafasi yake ya hapo awali kama OCPD wa Kaloleni.