Mbunge wa Mvita Abdulswamad Shariff Nassir amewataka viongozi walioasi chama cha ODM kujiuzulu mara moja na kusimama na chama walichohamia ili kukitetea kiti hicho.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza wakati wa hafla ya kusherehekea miaka kumi ya chama hicho katika bustani ya Mama Ngina, Abdulswamad alisema viongozi hao sharti wajiuzulu na sio kusubiri hadi mwaka 2017 ikizingatiwa kuwa wanawanyima wananchi wao uwakilishi kisawasawa.

Aidha amesema kuhama kwa viongozi hao hakumaanishi kuwa maeneo bunge yao ama kaunti zao zimehamia kwenye chama walichoenda akisema kuwa viongozi hao walikuwa wakishikiliwa na chama.

Wakati huo huo amewataka waasi hao kutorudi tena kwenye chama cha ODM kwa kuwa wataona mabadiliko wakati wa uchaguzi ujao.

Kauli yake imeungwa mkono na Seneta wa Siaya James Orengo aliyewakashifu viongozi wa ODM walioasi chama hicho na kujiunga na chama kipya cha Jubilee.