Kaunti ya Nairobi ni miongoni mwa kaunti zilizohusika pakubwa na udanganyifu katika mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne KCSE.
Akitangaza rasmi matokeo hayo siku ya Jumatano katika jumba la Mitihani House jijini Nairobi, waziri wa elimu alisema kuwa visa vya udanganyifu katika mtihani wa KCSE mwaka wa 2015 vilikuwa vingi zaidi ikilinganishwa na mwaka wa 2014.
"Kwenye matokeo ya mtihani wa mwaka wa 2015 kuliandikishwa 70% ya visa vya udanganyifu kote nchini huku takriban watahiniwa 5,101 waliokalia mtihani huo wakikosa matokeo yao kwa kuhusika na udanganyifu. Kaunti za Nairobi, Makueni na Meru ndizo kaunti zilizokuwa na visa vingi vya udanganyifu," alisema Matiang'i.
Matiang'i aidha alisisitiza kuwa kila mwanafunzi aliyehusika na udanganyifu ataadhibiwa kibinafsi na sio shule kwa ujumla.
Aidha Matiang’i amefichua kuwa Rais Uhuru Kenyatta amewaagiza mawaziri yeye pamoja na waziri wa usalama wa ndani Joseph Nkaissery kutoa ripoti ya uchunguzi wa wizi wa mtihani.
Kwa mujibu wa matokeo hayo thuluthi moja 1/3 ya watahiniwa walipata alama ya C+ kwenda juu alama inayowawezesha kujiunga na vyuo vikuu.
Somo la Kiswahili na Kingereza ni miongoni mwa masomo yaliyofanya vizuri huku somo la hisabati, historia, somo la dini na la kiisilamu yakitajwa miongoni mwa masomo yaliyofanya vibaya.