Kaunti ya Mombasa inatarajiwa kuzindua kamati itakayoharakisha shughuli ya usajili wa vitambulisho vya kitaifa.
Hatua hiyo inatarajiwa kuhakikisha wananchi wanajitokeza kwa wingi kujisajili kama wapiga kura wakati wa uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2017.
Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Maalim Mohamed amesema kuwa watashirikisha idara ya usajili wa watu pamoja na maafisa wengine wa serikali katika kamati hiyo ili kuhakikisha shughuli hiyo inafanikiwa.
Akizungumza na wanahabari ofisini mwake siku ya Jumatatu baada ya kukutana na mwenyekiti wa Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC Isaack Hassan, Maalim alisema kuwa ofisi yake itashirikiana kikamilifu na tume hiyo ili kuhakikisha uchaguzi mkuu ujao unafanikiwa.
“Vijana hawawezi kupiga kura iwapo hawana vitambulisho. Tunataka kuhakikisha vijana wanapata vitambulisho kwa haraka ili kupiga kura mwaka 2017,” alisema Maalim.
Haya yanajiri huku Kaunti ya Mombasa na eneo la Pwani kwa jumla likitajwa kuandikisha idadi ndogo ya wapiga kura kufikia sasa.