Rais Uhuru Kenyatta ametahadharisha walimu wakuu dhidi ya kufuja fedha zilizotengwa kutumika katika mfumo wa elimu ya bure.
Kenyatta alisema kuwa watakaopatikana na hatia watakachukuliwa hatua kali za kisheria na kuwataka walimu kuwajibika kazini.
Akiongea siku ya Jumatano baada ya kufungua rasmi kongamano la walimu wakuu jijini Mombasa, Rais Kenyatta alisema kuwa serikali ya Jubilee imeboresha sekta ya elimu kwa kuongeza fedha zilizotengewa sekta hiyo.
Asilimia 20 ya bajeti nchini imetengewa sekta hiyo.
Rais Kenyatta pia amewakashifu walimu ambao huwasaidia wanafunzi katika wizi wa mitihani na kusema kuwa serikali kupitia kwa Wizara ya Elimu imewasilisha mfumo mpya wa elimu ambao utahakikisha kuwa wizi wa mitihani unakabiliwa.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu Fred Matiang'i alisema kuwa changamoto inayokumba shule nyingi humu nchini ni ukosefu wa walimu wa kutosha na miundo mbinu.
Hata hivyo, aliwahakikishia walimu hao kuwa serikali imeweka mikakati ya kuwaajiri walimu zaidi.
Mwenyekiti wa muungano wa walimu wakuu nchini John Awiti kwa upande wake alitoa wito kwa Tume ya kuwaajiri walimu nchini TSC kuhakikisha kuwa mbinu wanazotumia kuwapandisha walimu cheo ni za halali.