Mwenyekiti wa shirika la watu waliothiriwa na ugonjwa wa haemophilia amewataka wazazi na wanao kupimwa ili kutambua iwapo wanaugua ugonjwa huo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Pauline Luvumbi, ambaye ni mwathiriwa wa ugonjwa huo, alisema kuwa baadhi ya watu wanaougua ugonjwa huu hujificha kutokana na uoga wa kutambulika iwapo wanaugua.

Ametoa wito kwa wazazi ambao watoto wao wameathirika na ugonjwa huo kujitokeza ili wapate matibabu badala ya kuwaficha nyumbani.

Aidha, Luvumbi ameitaka serikali ya Kaunti ya Mombasa kuweka vifaa zaidi vya kuhifadhi dawa maarufu kama 'freezer' katika kila zahanati.

Luvumbi alisema kuwa ugonjwa huo unaosambazwa kupitia urithi kutoka kwa mzazi hadi kwa mtoto, pia umeathiri wanawe wawili mmoja wa miaka 15 na mwingine 27, hali iliyomsababisha kuanzisha shirika hilo.

Haemophilia ni ugonjwa unaosababisha mtu kuvuja damu kwa wingi anapopata jereha na hata unaweza kusababisha kifo.

Ugonjwa huo, ambao una aina mbili, Haemophilia A na B, husababishwa na uhaba wa viwango vya chembechembe za kuzuia kuvuja kwa damu mwilini.