Wanaopenda kujadili siasa bila shaka hawawezi kubali siku kupita bila ya kutegea sauti hii inayopasua mawimbi kwa mijadala endelevu na komavu inayohusiana na siasa za Pwani.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Jina kamili ni Solomon Zully, Mwanahabari tajika kutoka kanda ya Pwani anayepeperusha kipindi cha kongamano kupitia idhaa ya Radio Salaam.

Kimtazamo hauwezi ukaamini kamwe jinsi anavyochambua na kudadisi mijadala ya siasa kuanzia kiti cha ugavana kwenda chini hadi mwakilishi wa wadi kila siku kuanzia saa mbili unusu usiku.

Zully ni mojawapo ya watangazaji wanaotegemewa kwa kiasi kikubwa na baadhi ya mashabiki wanaopenda siasa kutokana na uzoefu wake wa ufafanuzi wa sera za wanaogombea nyadhifa mbalimbali kutoka kaunti zote za Pwani.

Kando na maswala ya siasa, Zully ni mmoja wa watangazaji mahiri katika kituo hicho aliyejinyakulia tuzo chungu nzima.

Ametuzwa mara tatu kama mwanahabari bora na Baraza la waandishi wa habari hapa nchini.

Zully anakiri kupata uzoefu wake katika maswala ya siasa alipokuwa mtoto mdogo baada ya kupenda kujadili kitu kidogo kwa mapana na kutoa mifano wazi katika jamii.

Alisema alipojiunga na kituo hicho, hakusita kueleza ari yake kwa muhariri mkuu kuhusiana na mwito aliokuwa nao katika maswala ya siasa.

Alipewa nafasi ya kufundishwa namna ya kuandika taarifa za kiasiasa na hivyo ndivyo alivyoishia kutambua njia mbalimbali za kuandika habari za siasa.

Kwa sasa, Zully ni mwandishi na muhariri mkuu wa habari za siasa katika kituo hicho ambacho alisema kimemkuza katika tasnia hii ya uandishi wa habari.