Wanawake wawili wanaodaiwa kuwahifadhi washukiwa watatu wa ugaidi waliovamia Kituo cha polisi cha Central watazuiliwa korokoroni kwa siku 20, huku mwenzao akizuiliwa kwa siku 30 wakisuburi uchunguzi kukamilika.
Hakimu Emmaunel Mutunga ameagiza Naima Mohammed Abdi na Shukri Ali Hajj kuzuiliwa kwa siku 20, na mshukiwa wa tatu Saida Ali Hajj kwa siku 30.
Haya yanajiri baada ya mwendesha mashtaka Eugine Wangila kuiambia mahakama kuwa wanahitaji muda wa siku 30 kukamilisha uchunguzi.
Aidha, Wangila alisema polisi wanahitaji muda wa kuchunguza jinsi watatu hao ambao ni raia wa Somali waliwasili humu nchini.
“Washukiwa hao ni raia wa Somali, hivyo tunataka kusafiri hadi nchini humo kuchunguza vipi waliweza kuingia Kenya,” alisema Wangila.
Hatua hiyo ilipingwa na Jackson Wachira, wakili wa washukiwa hao aliyesema kuwa madai yanayotolewa na afisi ya mashataka ya umma si ya kweli.
“Hakuna sababu mwafaka ya kuwazuia wateja wangu kwa sababu ni haki yao kikatiba kuwa huru,” alisema Wachira.
Katika kesi nyingine, wasichana watatu walifikishwa mahakamani baada ya kuhusishwa na shambulizi hilo la Kituo cha polisi cha central.
Nastaheno Ali Thalili, Luul Ali Thahil na Zamzam Abdi Abdallah walitiwa mbaroni mnamo Septemba 19 na 20, kwa tuhuma za ugaidi na kuwa na ufahamu na shambulizi hilo.
Watatu hao wanadaiwa kuwa marafiki na washukiwa waliouawa baada ya shambulizi hilo kutibuka.
Kiongozi wa mashtaka Erick Masila aliiambia mahakama kuwa polisi wanahitaji muda wa siku saba kuchunguza simu za washukiwa hao, kabla ya kuwafungulia mashtaka.
Ombi lililopingwa na wakili wa washtakiwa hao Jerad Magolo aliyesema kuwa hakuna sababu mwafaka ya kuwazuia wateja wake.
Magolo ameongeza kuwa hatua hiyo inakiuka haki za mshukiwa kulingana na katiba.
Aidha, amesema kuwa madai ya kuwa wateja wake walikuwa na urafiki na washukiwa hao wa ugaidi haliwezi kuwa sababu ya kuwazuia kwa muda zaidi.