Mkuu wa huduma za mauzo katika kampuni ya KIWASCO amesema kuwa kampuni hiyo imefanikiwa kusambazia asilimia 68 ya wakaazi wa Kisumu maji safi.
Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatatu, Thomas Odongo, alisema kuwa kampuni hiyo iko kwenye harakati za kuweka mikakati mwafaka zitakazowawezesha kuimarisha huduma zao, kama njia mojawapo ya kuhakikisha wakaazi wananufaika na maji safi.
Odongo alisisitiza kuwa lengo kuu la KIWASCO ni kuona kuwa kila mmoja katika jamii anazingatia matumizi ya maji safi.
“Nawashauri wakaazi wa Kisumu ambao hawana maji ya mfereji kufika katika afisi zetu ili kupokea huduma hizo,” alisema Odongo.
Aidha, alisema kuwa KIWASCO imepanua huduma zake katika maeneo mbalimbali ikimwemo maeneo ya Airport na Miwani, miongoni mwa maeneo mengine.
Hatahivyo, alisema kutokana na hatua ya vyanzo vingi vya maji kuchafuliwa katika Kaunti ya Kisumu, kampuni hiyo ya KIWASCO imelazimika kutumia kemikali nyingi zaidi kutibu maji inayosambazia wateja wake.