Tamasha la sherehe za utamaduni wa Lamu zilianza mapema Alhamisi.
Sherehe hizo ambazo hufanyika kila mwaka huvutia wageni kutoka sehemu mbalimbali, ikiwemo ndani na nje ya nchi.
Mbwembwe na furaha zilitanda kwenye siku ya kwanza ya hafla hiyo huku mashindano ya uvuvi wa samaki yakivutia mashua 43.
Mashindano hayo yalianza alfajiri na kukamilika alasiri ambapo mashua 29 zilimudu hadi mwisho.
Katika kundi A, sulisuli wa kilo 28 alipatikana huku kwenye kundi B, tewa wa kilo 16 alivuliwa.
"Tueleze maoni yako kuhusu sherehe hizi za Lamu"
Nayo mashindano ya jahazi yalivutia washindani 10 ikiwa ni jahazi kutoka Patte, Kizingitini na Matondoni.
Jahazi Alburaq ya Patte ilitwaa ushindi ikifuatiwa na Intiswam ya Kizingitini na ya tatu ikiwa ni Firdaus ya Patte. Washindi wote watatangazwa na kupokea zawadi zao hapo Ijumaa (Novemba 23).
Naye afisa mkuu wa Idara ya Biashara kwenye kaunti ya Lamu Twaa Salim alifungua rasmi mchuwano wa soka ya ufukweni katika ufuo wa bahari ya Shella.
Mchuwano huo unajumuisha timu kutoka mji wa Kizingitini, Shella, Faza na Mkomani ikiwa ni miongoni mwa sherehe za tamasha za utamaduni wa Lamu.