Hisia mseto zinazidi kuibuka nchini baada ya aliyekuwa katibu wa Chama cha ODM Ababu Namwamba kutangaza kuongoza Labour Party iliyozinduliwa upya siku ya Alhamisi.
Wengi wametaja uamuzi wa Ababu kutetea kiti chake cha ubunge Bundalangi kupitia chama hicho ambacho kimekuwa chini ya uongozi wa Prof Julia Ojiambo kama hatua isiyokuwa na msingi, ikizingatiwa kuwa chama hicho hakina uungwaji mkono wala ushawishi wa kutosha kisiasa.
Vincent Mwachiro ambaye ni katibu mkuu wa Baraza la wazee wa jamii ya Mijikenda amesema kuwa Ababu ameteleza kisiasa na huenda akapoteza umaarufu wake.
Mwachiro alisema kuwa Ababu alipokuwa upande wa upinzani alikuwa na umaarufu kutokana na kupata uongozi kutoka kwa kinara wa upande wa upinzani Raila Odinga.
“Hatua aliyochukua Ababu ya kumsaliti baba wake wa kisiasa Raila Odinga ilikuwa hatua ambayo haistahili,” alisema Mwachiro.
Hata hivyo, Mwachiro alisema kuwa umaarufu wa Ababu utarudi iwapo atarudi kwa chama cha ODM ama kujiunga na Chama kipya ya Jubilee.
Aidha alisema kuwa iwapo mbunge huyo atasalia katika Labour Party, basi asahau ubunge.