Katika juhudi za kuwaweka wanafunzi masomoni au katika shughuli mwafaka zinazoambatana na maswala ya uwajibikaji katika Jamii, sasa Mbunge wa Mvita Abdulswamad Shariff Nassir amewasihi wanafunzi wa kaunti ya Mombasa kuhudhuria masomo ya ziada ya bure katika shule ya kibinafsi ya Istiqama mjini humo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza baada ya kufungua rasmi masomo hayo mjini Mombasa siku ya Jumamosi yanayowajumuisha wanafunzi katika kidato cha tatu na cha nne na wale wa darasa la nane, Abdulswamad amesema kuwa masomo hayo yana umuhimu mkubwa kwa wanafunzi kwani yatawasaidia kuimarika kimasomo.

Abdulswamad amesema kuwa mara nyingi wanafunzi wengi husalia nyumbani wakisubiri shule zifunguliwe ilhali ni kupitia kwa masomo kama hayo ndipo wanafunzi hao watadurusu vitabu vyao na kufanya vyema katika mitihani ya kitaifa na maisha yao ya baadaye.

Mbunge huyo wa Mvita amesema kuwa atawazawadia wanafunzi watakaohudhuria mafunzo hayo ya bila malipo ili kuwatia motisha wanafunzi wengi kuthamini masomo na wamefaulu maishani.

“Nimeanzisha mpango huu kuwasaidia wanafunzi kufanya vyema katika masomo yao wakati wa mitihani ya kitaifa na pia maisha yao ya baadaye,” alisema Abdulswamad.