Share news tips with us here at Hivisasa

Idadi kubwa ya abiria mjini Kisii wamelalamikia ongezeko la nauli hasa kufuatia kufunguliwa kwa shule kwa muhula wa tatu.

Abiria hao walisema kuwa imekuwa mazoea kwa wahudumu wa magari mjini Kisii kupandisha nauli bila kufuata utaratibu unaofaa wakati wateja wanapoongezeka.

Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumanne katika kituo cha magari mjini Kisii, abiria hao walisema wameongezewa nauli kwa kiasi kilicho juu zaidi jambo ambalo wamekerwa nalo.

Abiria hao wameiomba idara husika kuwajibika kwa kuingilia kati na kuwasaidia kwani nauli imepandishwa sana.

“Inaonekana kuwa biashara hii imenoga kwasababu wahudumu wa magari wameanza kuongeza nauli katika maeneo mbalimbali nchini, Kisii ikiwa moja wapo,” alisema Hesbon Kamanda, abiria.

Wasafiri wengi katika kaunti ya Kisii kwenye barabara ya kutoka Kisii kuelekea Miruka, Kisii-Nyamira, Kisii-Nyamache wamesema kuwa wanalipa nauli isiyokuwa ya kawaida, baada ya wanafunzi kuanza kumiminikia katika vituo hivyo vya magari.

Abiria hao wamesema nauli inafaa kupanda iwapo bei ya petroli na diseli imetangazwa kupanda nchini, wala sio kupandisha bei kiholela.

“Tumeshindwa kujua kwa nini wahudumu hawa wanapenda kuongeza nauli bila kufuata utaratibu wa kiuchumi. Hali hiyo inatudhulumu sisi kama abiria,” alisema Joyce Obiero, abiria

Wafanyibiashara wanaoendesha biashara yao mjini Kisii na wanatoka katika maeneo ya Kegogi, Nyamira na maeneo mengine wamesema hali hiyo inawaathiri sana kiuchumi na kuomba usaidizi.