Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Evans Achoki amewahakikishia watalii kuwa usalama umeimarishwa katika kivuko cha feri cha Likoni na eneo la Mji wa Kale.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Achoki amepuzilia mbali agizo la Marekani la kuwataka raia wake kutotumia kivuko hicho cha feri pamoja na kutembelea Mji wa Kale hasa wakati wa usiku.

“Kila mgeni na raia wa taifa hili amehakikishiwa usalama. Watalii wote wako huru na salama kutumia kivuko cha feri wakati wowote,” alisema Achoki.

Kamishna huyo amesisitiza kuwa idara ya usalama iko tayari kukabiliana na visa vya ugaidi wakati wowote ule.

“Polisi wako imara kila wakati na tutapambana na magaidi ambao wanataka kutatiza usalama wa taifa,” alisema Achoki.

Wakati huo huo, amemtaka Gavana wa Mombasa Hassan Joho kuripoti kwa polisi iwapo usalama wake uko hatarini badala ya kulalamika majukwaani.

Ameongeza kuwa serikali haina njama ya kumua gavana huyo kama inavyodaiwa.

“Hatuna njama ya kumuangamiza Joho wala kiongozi yeyeto yule. Serikali inalinda na kujali usalama na maisha ya kila kiongozi na Mkenya,” alisema Achoki.