Kamishna wa Mombasa Evans Achoki ametoa wito kwa wachungaji kutuma maombi kwa idara ya polisi ili wapewe ulinzi wakati wa ibada.
Kamishna huyo ametoa hakikisho kwa wachungaji hao kwamba idara ya polisi iko tayari kuhakikisha kuwa waumini wanaendeleza ibada zao bila uoga wa kuzuka kwa mashambulizi.
Akiongea siku ya Jumapili katika kanisa la Joy in Jesus lililoshambuliwa na magaidi miaka miwili iliyopita huko Likoni, Achoki alisema watahakikisha tukio kama hilo halitokei tena.
Alitaja tukio hilo kama baya zaidi na kusema njia ya kipekee ya kuzuia jambo kama hilo kutokea tena ni wachungaji wa makanisa kushirikiana kwa karibu na idara ya polisi.
Licha ya kwamba shambulizi hilo lilitokea miaka miwili iliyopita, baadhi ya waumini wa kanisa hilo walisema kuwa bado wao huwa na wasiwasi kila wanapohudhuria ibada ya Jumapili.
Baadhi ya makanisa katika eneo hilo pia yameshuhudia idadi ya waumini kupungua kutokana na wasiwasi.
“Ningependa kuwahimiza wakaazi wa Mombasa kuunga mkono mpango wa Nyumba Kumi ili kudumisha usalama katika maeneo wanayoishi,” alisema Achoki.