Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Evans Achoki ameyaonya makundi ya vijana na wanawake dhidi ya kutumiwa na wanasiasa kuzua vurugu wakati wa mikutano.

Share news tips with us here at Hivisasa

Achoki amesema hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya makundi hayo.

“Tutawakabili vilivyo iwapo hawatakoma kuzua vurugu katika sherehe za kiserikali na mikutano mingine ya siasa,” alisema Achoki.

Kauli hii inajiri baada ya vurugu kuzuka wakati wa sherehe za sikukuu ya Jamuhuri katika uwanja wa Tononoka.

Wafuasi wa Gavana wa Mombasa Hassan Joho na wale wa Mbunge wa Nyali Hezron Awiti walirushiana maneno na kutatiza hotuba ya rais iliyokuwa ikisomwa na kamishna Achoki.

Akizungumza afisini mwake, Achoki alisema hakuna mtu yeyote aliyetiwa mbaroni, na kuongeza kuwa iwapo wanawake hao watazua vurugu tena, basi watakabiliwa na mkono wa sheria bila ya kujali jinsia zao.