Mkurugenzi katika Wizara ya Mazingira kutoka Kaunti ya Kisii Samson Bokea amedai kuwa kwa muda wa miaka kumi ijayo sehemu ya Gusii inahofiwa kukumbwa na ukosefu mkubwa wa maji.

Share news tips with us here at Hivisasa

Bokea akiwa kwenye kikao muhimu alichokiandaa kuwaarifu wanahabari kuhusu athari za upanzi wa miti inayojulikana kama Eucalyptus kando ya mito ni tishio kubwa kwani mti huo huenda ukamaliza maji ya mito katika maeneo hayo.

Bokea pia amesema kuwa shughuli za kibinadamu zinazoendelezwa karibu na mito ndizo zimechangia sana shida za kukosa maji.

Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa upanzi wa miti ijulikanayo kwa jina la kisayansi Eucalyptus ambayo inajulikana kwa kuvuta maji mengi karibu na mito au chemichemi za maji haifai kupandwa haswa kando ya mito au karibu na visima.

"Mti mmoja wa Eucalyptus unatumia takriban lita mia mbili za maji kwa siku moja peke. Sasa ikiwa mkulima amapanda miti mia tano kando ya mto, ni siku au miezi au miaka mingapi itakayopita kabla mto huo kukauka?,” aliuliza huku akiwashauri wakulima na wawekzaji katika sekta ya upasuaji mbao kupanda aina tofauti ya miti ambayo hautaathiri kiwango cha maji mitoni iwapo itapandawa kando ya mto.

Afisa huyo amewarai wakaazi wa sehemu ya Kisii kukomesha kwa dharura tabia hiyo ya upanzi wa miti kando ya mito, akisema kwamba tatizo hilo lina uwezo wa kuigeuza sehemu hiyo kuwa nchi kavu isiyokuwa na mito wala chemichemi za maji katika siku zijazo.

Kando na kuipanda miti hiyo karibu na mito, Bokea pia amewaomba wenyeji wa eneo hili kukoma kulima hadi kando ya mito na pia kutafuta njia ya kuyateka na kuyahifadhi maji hasa yale ya mvua  ambayo pia ni mazuri kwa matumizi ya nyumbani la sivyo wajiandae kwa msimu mrefu wa ukame katika maeneo hayo.