Mbunge wa Mvita Abdulswamad Sharriff Nassir amejitokeza na kupinga vikali tendo la kuwanyima fursa ya kusali vijana watatu waliokamatwa kwa tuhuma za ugaidi.
Akizungumza mjini Malindi baada ya kushuhudia kuachiliwa kwa watatu hao, mbunge huyo alitoa wito kwa serikali kumchukulia hatua afisa wa polisi aliyehusika na jambo hilo.
"Idara ya Polisi yapaswa kumchukulia hatua za kinidhamu polisi aliyewanyima vijana hao fursa ya kufanya ibada yao," alisema Abdulswamad.
Kwa mujibu wa kituo cha redio cha Milele, mbunge huyo pia aliwakosoa polisi na kuwaambia wasiwakamate wananchi kiholela.
Idara ya Polisi Malindi iliwaachilia vijana hao watatu pasipo na masharti huku watatu hao wakidai kuwa bado hawakufahamu sababu za kukamatwa kwao.