Siku ya Mayatima Duniani iliadhimishwa huku wito ukitolewa kwa viongozi na jamii kuwa waaminifu katika ndoa na kuwajali watoto ambao hawana wazazi kwa kuwapeleka shuleni.
Maadhimisho hayo yalifanyika siku ya Alhamisi katika Shule ya Msingi ya Iterio, Suneka katika Kaunti ya Kisii, ambayo yalifana mno, huku wanafunzi kutoka Shule mbali mbali wakiwaburudisha wageni waliohudhuria hafla hiyo kwa ughani wa mashairi, nyimbo na michezo ya kuigiza ambayo iliangazia umuhimu wa kuwajali mayatima.
Akihutubu katika hafla hiyo, Afisa wa watoto katika Kaunti ya Kisii Joyce Keno aliwasihi wakaazi wa Gusii kujukumika katika kuwalea watoto mayatima na kuwaelimisha ili kuwa na jamii ya maendeleo katika siku za baadaye.
"Kila mmoja wetu sharti akumbuke asiyekuwa na mzazi mmoja au wote maanake tunapofanya hivyo tunapunguza watoto wa kurandaranda mitaani na mnajua ukimbagua yatima hana pa kuenda mbali na kuenda kuwa Chokora," alishauri Keno.
Aidha Afisa huyo wa watoto aliwashauri wote waliohudhuria maadhimisho hayo kuwa waaminifu katika ndoa na kuwataka vijana kupunguza uasherati ambao alisema umechangia pakubwa kuleta ugonjwa hatari wa ukimwi ambao umechangia uwepo wa mayatima wengi nchini kwa kiwango cha asilimia 48 kwa mia.
Naye Mwenyekiti wa Mandeleo ya Wanawake katika Kaunti hiyo Alphonsina Tebo aliwarai wazazi kuthamini ndoa na kuepukana na ‘Mpango ya kando’ ambao alisema umeleta magonjwa ya ukimwi na kuuwa idadi kubwa ya wazazi na kuacha watoto kuwa mayatima.
Miongoni mwa Shule zilizotia nakshi hafla hiyo ni Shule ya Upili na ya Msingi ya Iterio, Ekerubo Boarding, Shule ya Msingi ya Nyamokenye miongoni mwa nyingine.