Afisa mmoja wa Benki ya Dunia (World Bank) Charles Mochama ameiomba Serikali ya Kaunti ya Nyamira kuwa na kikao na wakurugenzi wa viwanda vya majani chai katika Kaunti hiyo ili kutafuta suluhu ya wakulima wa majani chai kupata hasara kwa kutochukuliwa kwa majani chai yao katika vituo vya kupima majani hayo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza na Wandishi wa Habari siku ya Jumatano katika mji wa Nyamira, afisa huyo alisema kuwa wakulima wamepata hasara kubwa kwa kutochukuliwa kwa majani chai yao kutoka vituoni kwa wakati ufaao.

“Wakulima wa majani chai hawastahili kuendelea kupata hasara haswa baada ya kazi ngumu shambani. Majani chai yao yanastahili kupimwa kwa wakati ufaao ili kuepuka hasara,” alihoji Mochama.

“Wakulima wanapopeleka majani chai yao kwenye vituo hivi, kwa mara nyingi wanalazimika kusubiri kwa zaidi ya siku nne ili kupima majani hayo na hiyo ni hasara maanake baada ya siku mbili tatu, majani hayo yatakuwa yameanza kuharibika na kupunguza uzani,” aliongezea afisa Mochama.

Mochama pia amewaomba washikadau wote wa sekta ya majani chai kutafuta suluhu mwafaka kutokana changamoto ambazo wakulima hupitia.

“Wakulima wamelalamikia jambo hili hadi wamechoka. Naomba Serikali ya Nyamira na ile ya Kitaifa wapange mkutano na wakulima, wale makarani wa kupima majani chai, wasimamizi wa viwanda, wale wasimamizi wa sekta ya majani chai kutoka sehemu ya Nairobi hata wale wanaouziwa majani katika nchi za ng’ambo na wengineo ili wakulima wapate haki yao,” alidokeza Mochama.