Afisa wa elimu katika kaunti ya Kisii Tomson Ngariba ameomba wakaazi ambao wanaishi karibu na shule kuwajibika kwa usalama na kuwa macho kwa shule hizo kuhakikisha kuna usalama wa kutosha.
Akizungumza siku ya Jumanne katika shule ya wasichana ya Itibo katika kaunti ya Kisii wakati wa kuwazawadi wanafunzi waliofanya bora katika mtihani wa kidato cha nne mwaka jana, afisa huyo alisema kuwa ili kuwa na usalama kwa shule za eneo la Kisii, sharti wakaazi walio karibu na shule kuwajibika kwa usalama il kuzuia visa vya mashambulizi na mikasa ya moto.
“Naomba wale mko karibu na shule kuwa macho kwa usalama ili kuzuia visa vya mashambulizi na mikasa ambayo hutokea kwa, shule na hiyo itatusaidia pakubwa kuweka usalama kwa shule zetu,” alidokeza Ngariba.
Wakati huo huo, afisa huyo alisema makanisa na wawekezaji wengine kusimamia shule badala ya tume ya TSC, serikali na wazazi ndio huchangia kutofanya bora katika mtihani wa kitaifa.
“Sasa makanisa mnataka kufanya kazi ya waziri wa elimu, kazi ya tume ya TSC hiyo ni mbaya na mnachangia shule kutofanya vizuri katika mtihani, naomba muwe kando serikali isimamie shule pamoja na wazazi,” aliongezea Ngariba.
Afisa huyo alishangaa sana kwa nini jibu halisi halijapatikana kuhusiana na mikasa ya moto ambayo imekuwa ikiathiri shule za eneo hilo, baada ya kamati kuundwa kufanya uchunguzi wa mikasa hiyo.
“Sioni kazi ya kamati ambayo iliundwa kufanya uchunguzi wa mikasa ya moto katika kaunti ya Kisii, maana bado hatujapokezwa jibu,” aliongezea.