Mwanamme mmoja mwenye umri wa makamu anaendelea kuuguza majeraha hospitalini, baada ya kile kinadaiwa kuwa alilawitiwa na afisa mmoja wa GSU katika eneo la Subukia.
Mwanaume huyo, ambaye ni baba wa watoto wawili aliviambia vyombo vya habari kuwa alifanyiwa kitendo hicho cha unyama ndani ya choo siku ya Alhamisi usiku.
Alisema kuwa afisaa mmoja kutoka kambi ya GSU, Molo alimnunulia pombe aina ya 'Keg' kabla ya kumfanyia unyama huo.
Alisema kuwa baada ya tukio hilo aliwafahamisha wananchi waliokuwa karibu ambapo iliwalizimu kutumia nguvu kuingia katika kituo cha polisi cha Subukia ili kuandikisha ripoti ya mambo yalivyojiri.
"Nilipowajulisha wananchi kilichojiri, walielekea mpaka katika kituo cha polisi cha Subukia, lakini polisi walitaka kutuzuia lakini baadaye tuliingia na kuandikisha taarifa," mwaathiriwa alisema.
Inadaiwa kuwa hadi sasa mshukiwa angali huru licha ya mlalamishi kuandikisha ripoti na kufuatilia kesi hiyo Ijumaa asubuhi.
Hata hivyo OCPD wa Subukia Alex Ng’ang’a aliyezungumza na wanahabari, amesema kuwa uchunguzi wa kesi hiyo tayari umeanzishwa.
Mlalamishi aliweza kupelekwa kupokea matibabu katika hospital ya Subukia kabla ya kuhamishiwa katika hosptali ya jimbo ndogo la Nyahururu kwa huduma zaidi.