Afisa wa kilimo katika kaunti ndogo ya Molo, Ann Odhiambo, amewaomba wakulima kutochoma takataka kwenye mashamba yao katika nyakati za msimu wa Kiangazi.
Afisa huyo ametoa wito huu baada ya moto uliowashwa na wakulima katika eneo la Kibunja kuteketeza hecta kadhaa za msitu na kupelekea uharibifu mkubwa.
Akihutubia wakulima katika kaunti ndogo ya Molo, Odhiambo alisema kuwa idara ya kilimo haipendekezi wakulima kuchoma takataka mashambani akisema mkusanyiko wa kwekwe na magugu hutumika kutengeneza mbolea.
Aliwashauri wakulima kupunguza gharama kwa kutengeneza mbolea wenyewe akisema hatua hiyo itaongeza rutuba kwenye udongo, mavuno pamoja na mapato yao ya kila mwaka.
Afisa huyo amesisitiza kwamba mimea haipati virutubisho kwa mbolea za maduka pekee akisema upungufu wa madini ya nitrojen na fosiforasi hupelekea mimea kubadili rangi.
Alisema dalili hizo huonyesha upungufu wa virutubisho akisema ni lazima wakulima waweze kutatua tatizo hilo haswa iwapo mimea iko katika hatua za ukuaji.
“Ni lazima wakulima walishe udongo ili nao ulishe mimea yao. Sisi wakulima hukimbilia mbolea kwa maduka ya kilimo na huenda mbolea hiyo ikose kuambatana na udongo wetu. Lazima tuzingatie hatua kadha iwapo tunataka kupata mapato kutoka kwa mpango wa kilimo biashara. Tusipuuze ushauri wowote iwapo tunahitaji mazao kutoka kwa jasho letu,’’ akasema Odhiambo.
Alisema baadhi ya mimea inayokuzwa na wakulima katika kaunti dogo ya Molo haiwezi vumilia ukame, wadudu pamoja na magonjwa huku akiwataka wakulima kukubatia hatua za unyunyiziaji maji mashamba kwa mimea isiyostahimili kiangazi.
Aidha afisa huyo ametamatisha kwa kusema serikali pamoja na idara za kilimo zinaendeleza utafiti ili kubaini jinsi ya kukabiliana na ugonjwa wa mahindi (maize lethal nicrosis) ambao umepelekea kupungua kwa mavuno ya mahindi na kutishia usalama wa chakula nchini.
Ugonjwa huo uliadhiri zao la mahindi haswa mkoani bonde la ufa mwaka jana huku wakulima wakikadiria hasara kubwa.