Huku shule nyingi zikiwa zimefunga kwa muhula wa kwanza, afisa wa watoto katika kaunti ya Kisii Joyce Keno amewaonya wazazi kuepuka kuwatumia watoto wao vibaya wakiwa likizoni.
Kwenye mahojiano na mwandishi huyu, Keno alitahadharisha wazazi ambao wamekuwa na mtindo wa kuwatumia watoto wao kufanya biashara kwenye mitaa ya mu wa Kisii, ambapo ni kinyume na sheria inayodhibiti masilahi na mstakabali wa watoto.
“Sheria itawaandama na kuwashika wazazi ambao watapatikana na kosa hilo la kuwatumia vibaya watoto,” alihoji Keno, huku akifunua zaidi kuwa watoto wengine hutumiwa kusambaza dawa za kulevya mitaani, hivyo basi kuweka hatima ya watoto hao kwenye hatari ya kupotoka kimaadili.
Aidha, alidokeza kuwa atafuatilizia visa ambavyo vimeripotiwa kwenye ofisi yake miongoni mwao mkiwa na watoto ambao wamekuwa wakionekana kando ya barabara moja ya kaunti ya Kisii wakiuza machungwa, na kuonya vikali kuwa wazazi ambao wamekosa kuwajibika sheria itafuata mkondo wake.
Afisa huyo amesema kuwa amekuwa akishughulikia visa vingi vya watoto ambao wameachwa na kutupwa mitaani, wazazi wanaotalikiana pamoja watoto wa kuzurura mitaani maarufu kama chokoraa ambao anadai wamekuwa wakiongezeka kwa kiwango kikubwa kwenye kaunti ya Kisii.
Aliwataka wazazi kuwa makini sana hasa wakati huu wa likizo, na kuwajibikia majukumu yao ipasavyo.
Aliongezea kusema kuwa iwapo ni kuwawajibisha watoto wao, iwe kazi ndogo ndogo za nyumbani bila kusahau kazi za kimasomo.