Afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma imekata rufaa katika Mahakama Kuu ya Rufaa kupinga dhamana ya Haniya Saggar, mke wa marehemu Sheikh Aboud Rogo.
Saggar na wasichana wengine watatu wanakabiliwa na madai ya kukosa kutoa ripoti kuhusu uvamizi wa Kituo cha polisi cha Central.
Mwendesha mashtaka Daniel Wamosa, kutoka afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma tawi la Mombasa, amesema anapinga dhamana ya shilling milioni moja, iliyopewa Bi Saggar.
Akizungumza siku ya Jumatano, Wamosa alisema Mahakama ya Shanzu haikuzingatia uzito wa kesi hiyo ilipokuwa ikitoa dhamana hiyo.
“Mahakama ya Shanzu haikutilia maanani uzito wa madai ya ugaidi yanayomkabili Haniya na wenzake watatu,” alisema Wamosa.
Rufaa hiyo inatarajiwa kusikizwa na jopo la majaji zaidi ya wawili katika Mahakama Kuu ya Rufaa.
Rufaa hii inajiri baada ya mahakama kuu wiki iliyopita kutupilia mbali ombi la awali la kusimamisha dhamana hiyo.
Jaji Dora Chepkwonyi alisema Saggar ataachiliwa kwa dhamana aliyopewa, iwapo afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma itakosa kukata rufaa.
“Iwapo siku saba zitapita basi mshukiwa huyo aachiliwe kwa dhamana,” alisema Jaji Chepkwonyi.
Jaji Chepkwonyi alisema kamwe hawezi kupinga uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Shanzu kuhusu dhamana hiyo.
“Mahakama ya Shanzu ilitekeleza jukumu lake kikataba, na siwezi kuingilia uamuzi huo kamwe,” alisema Jaji Chepkwonyi.
Saggar, Nastaheno Ali Thalili, Luul Ali Thahil na Zamzam Abdi Abdallah wanadaiwa kukosa kutoa habari kwa polisi kuhusu uvamizi wa Kituo cha polisi cha Central.