Mahakama ya Mombasa imeipa afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka siku saba kuwasilisha nakala za mashahidi wawili wa mwisho kwenye kesi ya ugaidi ya vijana wanane walionaswa katika msikiti wa Sakina.
Ali Kashimini, Alihaji Mohamed, Kazungu David na wengineo walitiwa mbaroni mnamo Novemba 17 mwaka 2014, katika msikiti wa Sakina wakiwa na gurunedi tatu, mapanga, visu na bunduki.
Agizo hili linajiri baada ya afisi ya mwendesha mashtaka ya umma tawi la Mombasa, kukosa kuukabidhi upande wa utetezi nakala hizo za mashahidi.
Akitoa agizo hilo siku ya Alhamisi, Hakimu Edger Kagoni alisema kuwa iwapo upande wa mshataka utakosa kuwasilisha nakala hizo kwa muda wa siku saba, basi mahakama itatoa uamuzi wa kufungwa kwa kesi hiyo.
“Iwapo mwendesha mashtaka hataukabidhi upande wa utetezi nakala hizo kwa muda ufao, basi mahakama itatoa mwelekeo wake wa mwisho,” alisema Kagoni.
Kesi hiyo itatajwa Agosti 29, 2016 ili kuthibithisha iwapo afisi ya mkurungenzi mkuu imewailisha nakala hizo za mashahidi kwa upande wa utetezi.