Mahakama kuu imetakiwa kuwaongezea dhamana wafanyakazi wanane wa Bandari ya Mombasa, Shirika la ukadiriaji ubora Kebs, na Halmashauri ya ukusanyaji ushuru nchini KRA, wanaokabiliwa na kosa la udanganyifu na wizi wa makasha.
Afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma tawi la Mombasa, imekata rufaa kutaka kuongezwa dhamana kwa wafanyakazi hao walioachiliwa kwa dhamana ya shilingi elfu 50, ama shilingu elfu 10 pesa taslimu.
Siku ya Jumatatu naibu mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma Alexendra Muteti alisema dhamana hiyo waliyopewa ni ndogo mno.
Hamisi Hemed Mwagarashi na wenziwe wanadaiwa kushirikiana na mfanyabiashara Abdulhafid Farah kukwepa ushuru wa shilling milioni 20, ambapo walisajili makasha yaliyokuwa na viatu vya wanawake kuwa yamebeba nguo kuu kuu.
Katika ripoti yake, KRA inaonyesha kuwa maafisa wa forodha waliidhinisha makasha 40,600 katika kipindi cha mwezi Juni na Julai, huku makasha 104 yakitolewa bila kulipiwa ushuru kisheria.
Kesi hiyo itasikizwa Septemba 13, mwaka huu.