Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Rais Uhuru Kenyatta amewaahidi wakazi wa Mombasa kuwa serikali itahakikisha kuwa soko la Kongowea linasafishwa na kufanyiwa ukarabati.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumanne jioni alipokutakana na mamia ya wakazi na wafanyibiashara wa soko hilo, Rais Kenyatta alisema kuwa tayari serikali imeweka mpango wa kusimamia shughuli za usafishaji wa soko hilo utakaoanza mwezi Februari mwaka huu.

‘’Tayari nimemuagiza waziri wa mambo ya vijana, akuje hapa na vijana wa NYS kutoka Nairobi washirikiane na vijana wa Mombasa, soko hili lisafishwe liwe katika hali nzuri ya kufanyia biashara,’’ alisema Rais.

Rais vilevile alisema kuwa serikali tayari imeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa soko hilo linafanyiwa ukarabati na kupanuliwa hadi kiwango cha kitaifa ili wafanyibiashara waweze kuendesha shughuli zao hadi nyakati za usiku.

Aidha, Kenyatta aliwahimiza wakazi kutokubali kuchochewa na matamshi ya baadhi ya wanasiasa, huku akiwataka kutokubali kugawanywa kwa msingi wa kidini, kisiasa wala ukabila.

‘’Wacha niwambie, msikubali kudanganywa na hawa wanasiasa, wakijaribu kuwadanganya wambie siku zao haziko mbali, mtawatupa nje katika uchaguzi ujao,’’ alisema Kenyatta.

Ziara ya Rais katika soko la Kongoweya huenda ikaleta afueni kwa wafanyibiasha ambao kwa muda sasa wamelalamikia kushuka kwa mapato kutokana na hali duni ya soko hilo.