Share news tips with us here at Hivisasa

Mahakama ya Mombasa imetoa agizo la kukamatwa kwa wafanyibiashara wawili wanaotuhumiwa kuingiza kemikali ya ethanoli nchini kinyume cha sheria.

Agizo hili linajiri baada ya naibu mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma tawi la Mombasa Alexendra Muteti kuwasilisha ombi la kukamatwa kwa Pius Kinywa na Mary Gathemia katika mahakama ya Mombasa, baada ya wawili hao kuenda mafichoni.

Muteti aliambia mahakama kuwa wawili hao hawajulikani waliko na inakisiwa kuwa walitoroka baada ya kusikia wanasakwa na polisi.

Pius Kinywa, Mary Gathemia ,Reuben Gachau na Hillery Bett, wanadaiwa kuingiza mitungi 800 ya ethanol nchini kupitia bandari ya Mombasa mnamo Februari 10, 2016, kinyume cha sheria, hatua iliyosababisha taifa kupoteza shilingi milioni 7.3 kama ushuru.

Kesi hiyo itatajwa Februari 23, 2016.