Wakaazi wa vituo vya kibiashara Subukia na Kabazi wamemtaka gavana wa kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua kutimiza ahadi ya kuweka mataa vituo hivo viwili.
Katika mahojiano na wakazi hao mwishoni mwa juma, wakaazi hao walisema mwishoni mwa mwaka jana, Mbugua aliahidi kuweka mataa hayo ya usalama kufanikisha lengo la uchumi wa masaa 24, lakini miezi tano baadae hilo halijatimizwa.
Akielezea hisia zake, mmoja wa wafanya biashara hao Njoroge Macharia alisema, “Sielewi ni kwa nini vituo vya kibiashara kama vile Maili Kumi, Bahati na Kiamaina vimewekwa mataa ya usalama, ilhali Kabazi na Subukia zingali gizani.”
Mwenzake Jane Wanjiku katika soko la Kabazi alisema watalazimika kungoja zaidi kuwekewa mataa hayo kwani kwa sasa ahadi hiyo imeonekana kama tabia ya wanasiasa kuwadanyanya wananchi.
Awali, waziri wa barabara katika serikali hiyo Maina Kairu kwenye ziara katika kituo cha kibiashara cha Subukia, alisema utengenezaji wa mataa hayo unafanyiwa nje ya nchi na kuwahimiza wakazi kuwa na utulivu.
“Serikali itatimiza ahadi yake ya kuweka mataa ya usalama sio tu katika kituo hicho cha kibiashara mbali pia vituo vingine,” alisema waziri huyo.
Mwakilishi wa wadi ya Subukia Peter Njoroge Mwanjo alisema anatoa msukumo kwa serikali ya kaunti kuweka mataa ya usalama kama ilivyo ahidi.