Maafisa wa NTSA katika oparesheni ya awali. [Picha/ nairobiwire.com]
Visa vya ajali za barabani katika ukanda wa Pwani vimepungua kwa asilimia 43 mwaka huu.
Haya ni kulingana na afisa mkuu wa halmashauri ya uchukuzi na usalama wa barabarani NTSA eneo la Pwani Ismail Farah.
Akizungumza na wanahabari jijini Mombasa, Farah alisema kupungua kwa ajali hizo kumetokana na kuwepo kwa maafisa wa NTSA barabarani.
Farah alisema kuwa juhudi za maafisa hao kuwachukulia hatua za kisheria wanaovunja kanuni za barabarani na kuwaelimisha madereva kuhusu nidhamu barabarani zimefua dau.
“Maafisa wetu wanafanya kazi yao vilivyo na watazidi kuwakamata madereva wanaokiuka sheria za barabarani,” alisema Farah.
Aidha, Farah amedokeza kuwa NTSA ina mipango ya kuanzisha matumizi ya leseni mpya ambayo itakuwa katika mfumo wa kielektroniki.
Alisema kuwa leseni hizo mpya zitarahisishia halmashauri hiyo kazi ya kufuatilia taarifa za magari kwa urahisi.
Aidha, alisema kuwa huduma hiyo itawawezesha kutambua aina za gari na jinsi zinavyoendeshwa kama njia moja ya kuzidisha usalama barabarani.
“Kupitia huu mfumo mpya wa leseni tutaweza kuwakamata madereva wakorofi,” alisema Farah.