Afisa mkuu wa idara ya trafiki katika mkoa wa Nyanza Joshua Omukata, amewarai wahudumu wa boda boda wawe waangalifu barabarani, ili kuzuia na kupunguza visa vya ajali.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kwa mujibu wa Omukata, watu zaidi ya 12 wamepoteza maisha yao katika eneo la Nyanza kwa kipindi cha chini ya juma moja, kutokana na ajali za pikipiki huku visa vingine vya ajali vikikosa kuripotiwa kwenye idara husika.

Katika mahojiano na mwanahabari wetu jijini Kisumu siku ya Jumatatu, afisa huyo wa trafiki alisema ajali hizo zinasababishwa kutokana na wahudumu wengi wa boda boda, kuendesha pikipiki kabla ya kuhitimu.

“Ukosefu wa pesa usije ukakufanya uangamie kwa sababu unataka upate pesa kwa kujiingiza kwenye biashara ya pikipiki na kisha baadaye uangamie,” akasema afisa huyo.

“Wakati utakapoumia, utatumia pesa zaidi kuliko ile shilingi hamsini ama mia moja ambayo ulikuwa unakimbia kwa kasi,”  alihoji Omukata.

Alitoa tahadhari kwa wazazi dhidi ya kuwaruhusu watoto wao hasa wanafunzi, kuendesha pikipiki wakati huu wa likizo, huku akiwaonya wahudumu hao dhidi ya kuendesha pikipiki kwa mwendo wa kasi.

Omukata alisema kuwa ni sharti waendeshaji wa pikipiki, wapokee mafunzo mwafaka ya kuwawezesha kumakinika barabarani, kwa usalama wao na vile vile usalama wa abiria wao.

Biashara ya boda boda inaendelea kunoga katika maeneo mbali mbali mkoani Nyanza, hasa wakati huu wa shamrashamra za Krisimasi na mwaka mpya.