Hali ya huzuni ilitanda katika eneo la Mtukanio 'B' kata ya Ndungiri, kaunti ndogo ya Nakuru kaskazini baada ya ajuza wa umri wa miaka 96 kujitoa uhai Jumatano majira ya asubuhi.
Akidhibitisha kisa hicho chifu wa kata hiyo Kabira Njine alidokeza kwamba ajuza huyo alijitoa uhai kwa kujinyonga kwa kamba ambapo mwili wake ulipatikana ukiniginia ndani ya chumba chake.
Kulingana na wakaazi , huenda mzozo wa kinyumbani ulipelekea nyanya huyo kujitoa uhai, tukio ambalo wamelitaja kama la kuhuzunisha kutokana na umri wake.
"Ni huzuni sana kuona mama mzee kama huyu akijitoa uhai. Kumekuwa na kutoelewana katika familia ya ajuza huyu na wanawe na tunashuku labda ndio ilipelekea yeye kujitoa uhai," alisema jirani mmoja ambaye alitaka jina lake kubanwa.
Chifu huyo hata hivyo alisema mwili wa mwendazake ulisafirishwa na maofisa wa polisi hadi hifadhi ya maiti ya hospitali ya mkoa mjini Nakuru huku uchunguzi kuhusiana na kisa hicho ukiendelea.