Wingu la simanzi lilitanda katika kijiji cha Kiambiriria katika tarafa ya Turi, baada ya ajuza mwenye umri wa miaka 74 kupatikana ameuawa kwa kupigwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia siku nya Jumamosi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Mwanamke huyo ambaye Jamaa zake wameeleza kwamba walikuwa wameriporti amepotea, wamesema walikuwa wanamtafuta tangu siku ya Alhamisi.

Aidha, wamesema kuwa wakiwa katika harakati za kumtafuta, walipokea habari kwamba kuna mama ambaye amepatikana ameuawa katika eneo la Kiambiriria viungani mwa mji wa Molo.

Mary Kagea, pamoja na mmoja wa ndugu zake amesema walipofika katika eneo la tukio, walipigwa na mshangao mkubwa baada ya kupata mwili wa mama yao kando ya barabara, huku maiti yake ikivuja damu baada ya kupigwa na watu ambao bado hawajajulikana.

“Kwa siku za hivi majuzi, mama amekuwa akichanganyikiwa kimawazo hadi akitoka nyumbani hawezi jua anakoenda ama anakotoka. Leo asubuhi tulipopokea habari kwamba kuna mwanamke amepatikana ameuawa, tukaamua kuja hadi eneo la mkasa na kinyume na matarajio yetu tukapata ni yeye,” alisma Kagea.

“Tuna huzuni isiyo na mfano kuona wahusika wameua mama yetu mzazi ambaye hakuwa na hatia,” akaongezea Kagea.

Chifu wa Kiambiriria Peter Muiruri, ambaye ameuliza wananchi kujiepusha na uvunjaji sheria amesema maafisa wa polisi wanaendelea kuchunguza mauaji ya mama huyo.

Mkuu wa polisi wilayani Molo Job Lesikinwa amewauliza wananchi kutoa habari kwa maafisa wa polisi ili wahusika wa mauaji hayo watiwe nguvuni.