Share news tips with us here at Hivisasa

Mwenyekiti wa kamati ya uhasibu wa pesa za umma kwenye Bunge la Kaunti ya Nyamira Ezra Mochiemo, amesema huenda akaunti za benki za maafisa wanaochunguzwa kuhusiana na madai ya ufisadi zikafungwa.

Akihutubu Afisini mwake siku ya Jumanne, Mochiemo alisema kuwa huenda kamati yake ikalazimika kuzifunga akaunti za benki za maafisa mbalimbali wanaochunguzwa na kamati yake.

Mochiemo alisema kuwa hatua hiyo itasaidia pakubwa kamati yake kufanya uchunguzi wake kwa uwazi, bila ya vikwazo vyovyote.

"Huenda tukalazimika kufunga akaunti za benki za maafisa waliohusishwa na ufisadi tunao wachunguza ili tusije tukaingiliwa kivyovyote na masuala yatakayo athiri uchunguzi utakao malizika hivi karibuni. Ningependa kuwaonya maafisa watakao jaribu kuficha pesa hizo kwenye akaunti tofauti," alisema Mochiemo.

Mochiemo aidha aliongeza kwa kuitetea hatua ya kuzifunga akaunti za benki za washukiwa wa ufisadi kwa kusema kuwa kufungwa kwa akaunti za washukiwa hadi uchunguzi utakapo tamatika hakutawanyima wahusika haki zao.

"Kuna baadhi ya maafisa tunao wachunguza ambao tayari wameiandikia kamati yangu barua za kututaka kutozifunga akaunti zao za benki. Kamati hii ina mamlaka ya kufanya hivyo kwa kuwa kazi yetu ni kuwachunguza. Akaunti hizo zitafunguliwa pindi tu uchunguzi utakapo tamatika," alisema Mochiemo.