Akina mama wachanga katika eneo la JC na Kiamaina kaunti ndogo ya Bahati Nakuru, wamesema wanakosa mabwana kwa sababu ya pombe haramu ambayo polisi wamekataa kupigana nayo.
Nao vijana wahudumu wa boda boda katika wadi za Kiamaina na Kabatini, wamelaumu polisi wa eneo hilo kwa kuwahangaisha pasi na sababu maalum, na kuwafungia katika kituo cha polisi cha Kiugu wakikosa kutoa hongo.
Wakizungumza na mwandishi huyu kwenye maandamano ya amani yaliyofanywa na wakaazi Ijumaa kufuatia kifo cha kijana wa miaka 23, walisema: “tunataka kwanza wote ambao wamefungiwa kwenye kituo hiki waachiliwe. Ukikamatwa hapa kwa kukataa kutoa hongo, unapelekwa mahakamani ukishinikiziwa kuuza bangi”.
Wakati wa maandamano hayo, mwakilishi wa wadi ya Kiamaina katika bunge la kaunti ya Nakuru Samwel Kamau, aliitaka idara ya polisi kuhamisha OCPD Duncan Nguthu na maafisa wake akisema wamekuwa wakiukaji wa haki za kibinadamu.
“Tunataka rais Uhuru Kenyatta aamrishe inspekta mkuu wa polisi joseph Boinnet, kuhamisha maafisa hawa kwa sababu wamekuwa kero kwetu. Wizi umeongezeka, hawafanyi kitu. Pombe wameshindwa kumaliza. Vijana wa bodaboda hawafanyi kazi yao kwa amani, sisi ni wakenya ama sisi sio wakenya?” Kamau alisema.
Hata hivyo polisi hao wakiongozwa na OCS David Rono walikataa kuachilia watu watatu waliokuwa wamezuiliwa kwenye kituo hicho wakati huo, wakisema walikamatwa kwa kuwa walanguzi wa dawa za kulevya.
Charles alikufa kwa kutumia pombe haramu.