Share news tips with us here at Hivisasa

Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae amewaomba akina mama wote katika Kaunti ya Kisii kutengeneza vikundi ili wakabidhiwe pesa za kufanya biashara ili kujiinua na kujiimarisha kimaisha.

Akiongea siku ya Jumanne katika uwanja wa shule ya msingi ya Tabaka iliyoko eneo bunge la Mugirango Kusini, Gavana Ongwae aliwaomba akina mama kujiunga kwa vikundi ili wakabidhiwe pesa za kufanya biashara kama njia moja ya kukuza biashara na kujiendeleza kimaisha.

“Najua akina mama wa kaunti hii wakipata pesa watajua jinsi ya kuzitumia. Naomba wasiokuwa katika vikundi muunde viikundi maana serikali yangu imetenga pesa ambazo tutawapa ili mfanyie biashara mpunguze umaskini katika kaunti yetu,” alisema Ongwae.

Akina mama ambao walikuwa kwa hafla hiyo walifurahishwa na matamshi ya Ongwae huku wengi wakisema watasaidika kupiitia kufanya biashara maana wengi hawana pesa za kuanzisha biashara hizo.

“Hii leo tutaunda vikundi tuende mpaka kwa ofisi ya gavana jinsi ametuambia ili tupewe pesa za kufanya biashara. Kitu ambacho kimekuwa changamoto kwetu sisi akina mama ni ukosefu wa pesa. Tungekuwa tumeanza biashara kitambo,” alisema Veronicah Moseti, mkaazi.

Aidha, Gavana Ongwae aliahidi kuleta maendeleo katika kaunti ya Kisii ili kutimiza yale aliyowaahidi wapiga kura wakati wa kampeini.

“Mwaka wa kwanza tulipoingia katika mamlaka hatukufanya maendeleo lakini mwaka wa pili tulianza kufanya maendeleo. Nitaleta maendeleo zaidi jinsi nilivyowaambia wakati nilikuwa nikitafuta kura,” aliongeza Ongwae.