Viongozi wa dhehebu la Akorino katika kaunti hii ya Nakuru, wanamtaka waziri wa elimu Fred Matiang’i kuwaadhibu walimu wakuu wanaowadhulumu wanafunzi wanaoshikilia imani yao.
Viongozi hao wakiongozwa na Gaitho Mbugua walionyesha kughadhabishwa kwao na ongezeko la visa vya wanafunzi kutoka dhehebu hilo wanaovaa kitambaa kichwani kudhulumiwa katika shule nyingi.
“Mara nyingi watoto kutoka dhehebu la Akorino hudharauliwa na walimu wakuu wa shule kiasi cha kuwafukuza shuleni na kuwadhulumu,” Gaitho alisema.
Walisema watoto wao huwa wanadhulumiwa kutokana na vitambaa hivyo.
Aliongeza kuwa baadhi ya shule zimekiuka katiba kwa kuwakataa watoto katika dhehebu hilo kusajiliwa katika shule hizo na hata wakati mwingine kuwapa adhabu kwa kuwafukuza shuleni.