Msanii tajika kutoka Tanzania Ali Kiba ameelezea jinsi alivyokwazwa katika tamasha la Mombasa Rocks, lilofanyika siku ya Jumamosi katika mkahawa wa Mombasa Golf club.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Ali Kiba ambaye aliimba nyimbo mbili katika tamasha hilo kabla ya kipaza sauti alichokuwa akitumia kukumbwa na hitilafu za kimitambo, alisema kuwa tukio hilo huenda lilifanywa kimakusudi ili kumharibia jina.

Akiongea na mtangazaji wa kipindi cha Mambo Mseto Willy M Tuva, Kiba hakusita kumkashifu meneja wa msanii Diamond Platinumz kwa madai kuwa alikuwa nyuma ya jukwaa alipokuwa akitumbuiza.

"Nilipokuwa nikitumbuiza nilimuona meneja wa Diamond akiwa nyuma ya jukwaa. Alikuwa anatafuta nini pale?” aliuliza Ali Kiba.

"Yeye anahusika kama nani pale? Hata kama watu wanafikiria kuna chuki kati yetu, haileti picha nzuri. Mashabiki watafikiria nini? Angekaa VIP atazame tamasha kama wengine lakini sio kukaa nyuma ya jukwaa,” aliongeza.

Hata hivyo, alisema kuwa hamaanishi kuwa meneja huyo alihusika moja kwa moja katika kitendo cha kipaza sauti kukumbwa na hitilafu.

Gavana wa Mombasa Hassan Joho hata hivyo alimuita Ali Kiba jukwaani baada ya Chris Brown na Wizkid kuondoka na kumpa nafasi ya kuwatumbuiza mashabiki wake.

Ali Kiba amewaomba radhi mashabiki wake na kuwaomba kuelewa tatizo halikuwa upande wake.