Aliyekuwa hakimu wa Mahakama ya Juu Jaji Samwel Oguk ameaga dunia.
Jaji Oguk alifariki katika Hospitali ya Aghakhan jijini Mombasa alipokuwa akipokea matibabu.
Akithibitisha kisa hicho siku ya Jumapili, mwenyekiti wa muungano wa wanasheria nchini tawi la Mombasa Benjamin Njoroge alisema kuwa jaji huyo alianguka na kuvunja mfupa ulioko karibu na kiuno siku ya Jumanne, na kufanyiwa upasuaji siku ya Ijumaa.
“Oguk alikuwa akionyesha ishara za kupata afueni baada ya upasuaji huo ila alizidiwa kiafya siku ya Jumamosi na kufariki,” alisema Njoroge.
Mwendazake amekuwa akifanya kazi ya wakili jijini Mombasa baada ya kustaafu kama hakimu wa mahakama kuu jijini Nairobi.