Aliyekuwa Spika wa Bunge la Kaunti ya Kisumu Anne Adul ametishia kuishtaki Tume ya Maadili na Kumbana na Ufisadi nchini (EACC), kwa madai kuwa tume hiyo ilichangia kumharibia jina kufuatia tuhuma za ufisadi zilizokua zikimkabili.
Akizungumza siku ya Jumatatu katika kikao na waandishi wa habari, Adul alisema kuwa kushtakiwa kwake mahakamani kuhusiana na madai ya kushiriki ufisadi kwenye bunge la Kaunti ya Kisumu, kulimharibia jina na hata kuikosesha familia yake amani na raha.
“Watu walio kwenye afisi kubwa kama vile EACC lazima wawajibike. Jina langu limepakwa tope kutokana na kupelekwa mahakamani bila sababu. Siwezi nikanyamaza. Lazima nitachukua hatua za kisheria dhidi yao,” alisema Adul.
Aliongeza, “Watoto wangu walipitia kipindi kigumu sana wakati jina langu lilipokua likipakwa tope kwenye vyombo vya habari.”
Hakimu wa mahakama kuu ya Kisumu Thomas Obutu alimwondolea lawama kufuatia tuhuma za kufuja pesa za bunge la kaunti ya Kisumu zilizokua zikimkabili.
Akitoa uamuzi huo, Hakimu Obutu alisema kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kudhibitisha madai dhidi ya Abdul.
Wengine waliondolewa mashtaka ya ufisadi ni Elijah Adul ambaye ni mumewe Anne, aliyekuwa kiongozi wa wengi Samuel Ong’owu, aliyekuwa kiongozi wa wachache katika bunge la kaunti hiyo Edwin Anayo na karani wa bunge hilo Nelson Sagwe.